Rapper na producer maarufu kutoka Marekani, Russ, ameweka wazi mtazamo wake kuhusu tatizo la msongo wa mawazo (depression) linalowakumba watu wengi, akisema kuwa mara nyingi chanzo chake ni kusahau kushukuru mafanikio ambayo mtu tayari ameyapata na badala yake kuangazia tu jambo moja ambalo bado halijatimia.
Akipitia mahojiano maalum na The Manager’s Playbook, Russ alisema:
“Watu wengi wanajikuta katika hali ya depression kwa sababu wanatupilia mbali mambo yote mazuri ambayo tayari wamefanikiwa na wanabaki kufikiria kitu kimoja tu ambacho hawajapata. Nami nilijikuta kwenye hali hiyo, lakini nilijifunza jinsi ya kutoka.”
Rapper huyo ambaye amejizolea umaarufu kwa muziki wake wa kujitegemea na mafanikio ya kujibeba binafsi bila msaada mkubwa kutoka kwenye lebo kubwa, alisisitiza kuwa shukrani ni silaha kubwa dhidi ya msongo wa mawazo. Alikiri kuwa hata yeye mwenyewe aliwahi kuingia kwenye hali hiyo, lakini alijifunza kutambua na kuthamini hatua alizopiga maishani.
“Nilikuwa na ndoto nyingi, baadhi hazikutimia kwa wakati niliotaka, na hapo ndipo nilianza kuona kana kwamba sijafanya chochote. Lakini ukweli ni kwamba nilikuwa tayari nimepiga hatua kubwa sana. Nilipoanza ku-appreciate hilo, hali yangu ilibadilika,Kutokuwa na shukrani ni kiungo kikubwa kuchochea msongo wa mawazo” alieleza Russ.
Kwa ujumla, Russ anatoa wito kwa watu kujifunza kuhesabu baraka zao, hata wanapokumbwa na changamoto, kwani kutokutimia kwa ndoto moja haifuti mafanikio yote mengine.