TIWA SAVAGE: NILIANZA MUZIKI BILA KUANGALIA PESA, LAKINI SASA NAJUA PESA NI KILA KITU

Mwanamuziki maarufu kutoka Nigeria, Tiwa Savage, amefunguka kuhusu safari yake ya muziki, akieleza kuwa alipoanza hakufikiria sana kuhusu fedha, bali aliingia kwenye muziki kutokana na mapenzi aliyonayo kwa sanaa hiyo. Hata hivyo, amesema kwamba kadri muda ulivyopita, aligundua kuwa pesa ni jambo la msingi sana katika muziki kuanzia kwenye promosheni, ujenzi wa chapa (branding), hadi mafanikio ya kazi kwa ujumla.

Akizungumza katika mahojiano maalum kupitia Kayafrica, Tiwa alisema:

“Nilipoanza, nilikuwa nataka tu kufanya muziki kwa sababu naipenda sana sanaa hii. Sikuwahi kufikiria kuhusu biashara nyuma ya muziki. Lakini baadaye nikagundua kuwa bila pesa, huwezi kusonga popote. Promo ni pesa, branding ni pesa, hata kupata nafasi sahihi ya kupiga show au kusikika kwenye media  vyote vinahitaji pesa.”


Tiwa Savage, ambaye kwa sasa ni miongoni mwa wasanii wakubwa na wenye ushawishi barani Afrika, alisema kuwa kuelewa thamani ya uwekezaji kifedha kwenye muziki kulimsaidia kubadilika na kujenga jina lake hadi kimataifa.

Kauli hii ya Tiwa Savage inakuja wakati ambapo wasanii wengi barani Afrika wanaendelea kutambua umuhimu wa biashara kwenye muziki, si tu kama kipaji bali kama sekta inayohitaji mikakati, mitaji, na weledi wa kibiashara ili kustawi.

Kwa sasa, Tiwa anaendelea kuachia Kazi na kushirikiana na majina makubwa duniani, huku akiendeleza harakati zake za kuinua vipaji na kuhamasisha wasanii chipukizi kutambua mapema thamani ya kuwekeza kwenye kazi zao.

  

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii