Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka China aliyeelezwa na polisi kuwa mmoja wa wanyanyasaji wa kijinsia wa kutisha zaidi nchini Uingereza amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Zhenhao Zou, raia wa China, aliwalewesha na kuwabaka wanawake watatu mjini London na wengine saba nchini China kati ya Septemba 2019 na Mei 2023.
Waendesha mashtaka wamesema kwamba watatu kati ya waathiriwa hao 10 wametambuliwa, lakini polisi wa Metropolitan wana hofu kuwa huwenda Zou alilenga wanawake wengi zaidi na wametoa wito kwa waathiriwa wengine waweze kujitokeza.
Tangu kesi hiyo kuanza, wanawake 24 wamejitokeza kutoa taarifa.
Wakati wa hukumu, Jaji Rosina Cottage KC alisema mshtakiwa ni kijana mwenye akili sana aliyekuwa akitumia sura ya ushawishi na haiba nzuri kuficha ukweli kwamba yeye ni mnyanyasaji wa kingono wa hatari.