NYOTA wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars, Ally Mayay Tembele, ametangaza rasmi nia ya kuwania nafasi ya Urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 16 Agosti 2025, jijini Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, mwakilishi wake anatarajiwa kuchukua fomu, ikiwa ni hatua rasmi ya kuanza safari ya kuwania uongozi wa juu wa shirikisho hilo linalosimamia maendeleo ya soka nchini.
Mayay, ambaye amewahi kuwa nahodha wa Taifa Stars na ni mmoja wa wachambuzi wa soka wanaoheshimika nchini, anaingia katika kinyang’anyiro hicho akiahidi kuleta mageuzi chanya katika uendeshaji na maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania.
Uchaguzi huu wa TFF unatarajiwa kuwa wa ushindani mkali huku wagombea mbalimbali wakijitokeza kuwania nafasi mbalimbali ikiwemo Urais na ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Kwa sasa Ally Mayay Tembele ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini.