Wanamuziki watano wauawa na wafanyabiasha wa dawa za kulevya

Wanamuziki watano wa bendi ya muziki ya Fugitivo nchini Mexico, waliotoweka tangu Jumapili, Mei 18, kaskazini mwa Mexico, waliuawa na washukiwa wa mauaji kutoka kundi la wafanyabiashara wa dawa za kulevya, mwendesha mashtaka wa jimbo la Tamaulipas amebainisha siku ya  Alhamisi.

Mwendesha mashtaka wa eneo hilo anashuku wafanyabiashara wa  dawa za kulevya kwa kuhusika na mkasa huo. 

Uchunguzi unaendelea kwenye eneo la tukio ili kubaini "mazingira ambayo wanamuziki wa bendi ya Fugitivo waliuawa," mwendesha mashtaka Irving Barrios amesema baada ya kupatikana kwa miili hiyo mitano.

Kulingana na uchunguzi, wanamuziki watano waliotoweka ni wanaume wenye umri wa kati ya miaka 20 na 40 kutoka bendi ya "Fugitivo" ambao walikuwa wameenda kwenye baa katika mji wa mpakani wa Reynosa siku ya Jumapili kucheza "Nortena," aina ya muziki kutoka eneo la jimbo moja la Mexico.

Watu wahujumiwa na mali kuporwa

"Uchunguzi umeendeshwa katika eneo ambalo miili mitano iligunduliwa, ambayo, kulingana na ripoti za awali, inaweza kuwa" ya wanamuziki hao watano, alielezea kwa undani msemaji wa Shirika la Usalama la Tamaulipas katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii. Taarifa kutoka kwa mwendesha mashtaka yenye maelezo zaidi kuhusu uchunguzi huo inatarajiwa "katika saa zijazo," ameongeza msemaji wa Tamaulipas, ngome ya magenge yenye ukatili zaidi (Los Zetas).

Wasanii hao walikodiwa kucheza kwenye ukumbi mmoja uliopo katikati mwa jiji la Reynosa, lakini walipofika, walikuta ni sehemu tupu, kwa mujibu wa familia zao, ambazo ziliripoti kutoweka kwao kwa mamlaka. Dada wa mmoja wa wanamuziki hao ambaye alikataa jina lake kutambuliwa kwa sababu za kiusalama, amesema alipokea simu za utapeli kufuatia kutoweka kwao. Pia aliripoti wizi wa magari mawili ya wanamuziki hao.

Wanafamilia hao, pamoja na wenzao wa bendi nyingine, walifanya maandamano Jumatano mbele ya makao makuu ya Jiji la Reynosa kabla ya kufunga daraja linalounganisha mji huo na mji wa Pharr, huko Texas. Wanamuziki wa Mexico wamekuwa walengwa wa vitisho kutoka kwa makundi ya wahalifu ambayo mara nyingi huwalipa ili kutunga na kuimba nyimbo za kusifu matukio ya viongozi wao, wanaojulikana kama "narcocorridos." Wasanii wengine mashuhuri wa kimataifa wa Mexico, kama vile bendi ya Los Ángeles Azules na bendi za miondoko ya Molotov na Café Tacvba, pia wamekuwa wakilengwa wa uhalifu, na vifaa na ala zao kuibiwa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii