Uongozi wa Klabu ya Simba umesema mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Yanga uliopangwa kufanyika Juni 15, 2025 upo kama ulivyopangwa.
Taarifa iliyotolewa kwa umma na uongozi huo imewataka wale ambao walinunua tiketi za mechi ya Machi 8, 2025 wazitunze kwa ajili ya matumizi ya mchezo huo na wale ambao hawajanunua tiketi wajiandae kununua baada ya tangazo la Bodi ya Ligi.
Aidha wamesema kuwa Inafahamika wazi kuwa Ligi Kuu ya NBC inajumuisha Timu 16 na si ligi ya timu moja, kwa mujibu wa taratibu kabla ya kuanza msimu vilabu vyote16 hushiriki vikao na kutoa mapendekezo ya kuboresha kanuni na taratibu ili kuimarisha ligi yetu, hivyo wenye hoja wafuate taratibu husika.
Hivyo wameiomba Bodi ya Ligi na TFF watoe hadharani ripoti ya uchunguzi juu ya wale wote waliohusika kuharibu mechi ya ligi jioni ya tarehe 7/3/2025 na wachukuliwe hatua stahiki na mamlaka husika.
Kutotolewa kwa ripoti na kutochukuliwa hatua kwa wanaoendelea kuchochea ghasia ni sawa na kulinda uharamia katika mpira ambao unatia dosari mafanikio yaliyopo katika tasnia ya mpira wa miguu nchini kwa sasa.