Uongozi wa Klabu ya Young Africans SC umetangaza rasmi kuwa hautashiriki mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Simba SC uliopangwa kufanyika tarehe 15 Juni, 2025.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo, Yanga SC imethibitisha kupokea barua kutoka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) tarehe 7 Juni 2025, ikiwataka kuhudhuria kikao maalum cha kujadili masuala yahusuyo mchezo huo (namba 184) unaotarajiwa kuzikutanisha timu hizo hasimu.
Klabu hiyo imesema ilitii wito huo na kushiriki kikao hicho kilichofanyika mapema leo asubuhi katika ofisi za Bodi ya Ligi zilizopo NSSF Mafao House jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Hata hivyo baada ya majadiliano ya muda mrefu viongozi wa Yanga waliwasilisha msimamo wao rasmi kwamba hawatashiriki mechi hiyo hadi pale matakwa yao ambayo tayari waliwasilisha kwa maandishi yatakapopatiwa majibu rasmi.
Yanga imewatakia heri Bodi ya Ligi pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kushughulikia matakwa hayo wakiwataka kulinda mustakabali wa maendeleo ya soka nchini.