Salah Vs Mane:Nyota wawili wa Anfield watamenyana katika AFCON leo, je ni nani atachukua kombe kati ya Cameroon na Misri?

Ni lala salama ya AFCON leo katika dimba la Olembe unaopatikana kwenye mji kuu wa Cameroon, Yaounde.Nyota wawili wa Anfield ya England watakutana kuoneshana ubabe katika mchezo unaotarajiwa kushuhudiwa na wapenda soka wengi ulimwenguni.

Senegal imetinga fainali ya pili mfululizo wakisaka taji la Afrika

na safari hii watavaana na Misri ambayo imekatia tiketi hiyo baada ya kuwasukuma nje wenjeji Cameroon kwa mikwaju ya penalti 3-1 katika hatua ya nusu fainali.

Na sasa fainali hii itakuwa ni ya nyota wawili wa kutoka Liverpool ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa tishio haswa kwa magolikipa wengi barani Ulaya.

Sadio Mane na Mohamed Salah ndio roho za timu zao wakiwa na mchango mkubwa mpaka kuzifikisha timu zao fainali.

Hadi wanafika fainali, Mane ambaye amecheza jumla ya dakika 520 kwenye michuano hiyo amechangia mabao matano, mwenyewe akifunga matatu na kutoa asisti mbili ikiwemo ya nusu fainali dhidi ya Burkina Faso na kuipa Senegal ushindi wa mabao 3-1.

Kwa Upande wa Mo Salah ambaye amecheza mechi zote kwa dakika zote 630 kwenye mashindano hayo, yeye amechangia mabao matatu akifunga mawili na kutoa pasi iliyozaa bao kwenye mchezo wao wa robo fainali dhidi ya Morocco.

Ugumu wa mpambano

Kwa vyovyote vile mechi hii itakuwa ngumu kwa timu zote mbili kutokana na timu zote kusheheni wachezaji wenye viwango vya juu na ukiangalia kuanzia kuanza kwa michuano timu hizo zimekuwa moto wa kuotea mbali.

Kutokana na kuwa na nyota wenye unyumbulifu mzuri lakini zaidi wanaocheza kitimu, wameweza kuwafikia hatua ya fainali bila ya kuwapo kwa alama ya kubebwa lakini pia wamekuwa tishio.

Senegal na Misri, wanaingia kwenye vita hii ya fainali huku wanaobashiri kwenye michezo ya kubahatisha wakiwa njia panda kujua yupi atashinda kutokana na uimara wa timu hizo.

Senegal

Kocha wa Senegal, Aliou Cisse ana kibarua kizito cha kufuta nuksi za Senegal kwenye michuano hiyo. Mwaka 2019, Senegal walipoteza mchezo wa fainali dhidi ya Algeria, lakini timu hiyo ilipoteza fainali ya mwaka 2002 wakati huo wakiwa na nyota kama; El Hadji Diouf, Henri Camara na Cisse ambaye ndio kocha wa sasa wa Simba ha owa Teranga.

Ama Senegal watwae kombe hilo kwa mara ya kwanza au Misri washinde kwa mara ya nane. Mmoja lazima aandike rekodi kwenye soka la Afrika hivyo mechi hiyo inarekodi ya aina yake na itakuwa ni mechi ya kusaka rekodi na heshima.

Rekodi za mabao Misri na Senegal

Kwa kuangalia rekodi zao kwenye michuano hii, basi unaweza kumpa ubingwa Senegal kwa kuwa wamekuwa vizuri zaidi baada ya kupita hatua ya 16 bora.

Misri wamefunga mabao manne tangu michuano ilipoanza ambapo kwenye hatua ya makundi walifunga mabao mawili kisha wakaweka kimiyani mawili dhidi ya Morocco kwenye robo fainali huku mechi ya nusu fainali dhidi ya wenyeji Cameroon wakipata ushindi wa penalti.

Kwa upande wa Senegal, baada ya hatua ya 16 bora wamefunga mabao nane ikiwa ni tofauti na hatua ya makundi walipofunga bao moja tu.

Mchezo huu ndio utaamua nani awe mchezaji bora wa michuano, nafasi zaidi kwa nyota Mane na Salah kutokana na kazi kubwa waliyoifanya wakishirikiana na nyota wengine kwenye zao.

Tuzo hiyo itaenda kwa yoyote kati ya hao kama tu timu yake itatwaa ubingwa kwani ubingwa ndio kigezo cha kumtwaa mchezaji bora na hii baada ya kumalizika kwa pambano hilo.

Safari zao mpaka fainali

Misri wakiwa kundi D la michuano hiyo, walimaliza nafasi ya pili wakiwa na pointi sita nyuma ya Nigeria waliokuwa na pointi tisa.

Baada ya kupita makundi, Misri waliwatoa Ivory Coast kwa changamoto ya mikwaju wa penalti 5-4, kisha robo fainali wakaifunga Morocco 2-1 na kumalizia kwa kuwatoa wenyeji Cameroon kwa penalti 3-1 kwenye mchezo wa nusu fainali.

Kwa upande wake, Senegal waliokuwa kundi B walimaliza kundi wakiwa ndio kinara wa kundi kwa kupata pointi tano. Waliwaondoa Cape Verde katika hatua ya 16 bora kisha wakawachapa Equitorial Guinea kwenye mchezo wa robo fainali na baadaye wakaiondoa Burkina Faso nusu fainali kwa kuwafunga mabao 3-1.

Mane, Salah wakiwa Liverpool wamekiwasha na rekodi zao ni za kutisha. Mane amecheza mechi 249 na kufunga mabao 103 huku akitoa asisti mara 37 katika rekodi zake za Ligi Kuu ya England, kwa upande wake Salah amecheza mechi 178 akifunga mabao 113 na kutoa asisti 43. Bila shaka fainali hii inayoshuhudia nyota hawa wakicheza timu tofauti kutamfariji kocha wa Liverpool, Jurgen Kloop.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii