Kisanduku Cheusi Ajali Ya Ndege iliyosababisha Vifo 67 Chapatikana

Mamlaka nchini Marekani zimesema zimefanikiwa kukipata kisanduku cheusi cha ndege ya abiria iliyogongana na helikopta ya kijeshi ya Black Hawk na kusababisha maafa makubwa.

Ajali hiyo imesababisha vifo vya watu 67 na kuingia kwenye historia ya kuwa ajali mbaya zaidi ya anga katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Ndege hiyo, mali ya Shirika la American Airlines, iligongana na helikopta ya jeshi wakati ikijiandaa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Ronald Reagan jijini Washington kisha kudondokea kwenye Mto Potomac.

Majina ya waliofariki katika ajali hiyo bado hayajatolewa lakini miongoni mwao, wapo vijana wadogo wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu (skaters) kutoka Kansas.

Seneta Maria Cantwell amesema miongoni mwa waliofariki pia wapo raia wa Urusi, Ufilipino, Ujerumani na China.

Kupatikana kwa kisanduku hicho cheusi, kunatarajiwa kutoa majibu ya haraka ya nini kilichosababisha ajali hiyo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii