Jeshi la Uganda, UPDF katika taarifa yake limesema litaimarisha ulinzi katika maeneo yake ya oparesheni hadi pale ambapo hali ya kawaida itakaporejea nchini DRC.
Kwa mujibu wa UPDF, hatua hii imechukuliwa kutokana na hali ya usalama kuendelea kuwa mbaya katika eneo la Kivu Kaskazini na maeneo jirani kutokana na mapigano kati ya wanajeshi wa serikali FARDC na waasi wa M23.
Aidha taarifa ya jeshi la Uganda inasema mpango huu unalenga kuzuia harakati za makundi mengine ya waasi yanayoweza kutumia fursa ya hali ya sasa kuendeleza agenda zao.
Aidha UPDF vilevile imesema hatua hii inalenga pia kulinda masilahi ya raia wa Uganda.
Mojawapo ya makundi ya waasi yanayoendeleza oparesheni zake mashariki ya DRC ni pamoja na waasi wa ADF ambao jeshi la Uganda kwa ushirikiano na lile la DRC yamekuwa yakipambana nalo tangu mwaka wa 2021 mwezi Novemba chini ya oparesheni iliyopewa jina la Shujaa.
Kulingana na UPDF, itashirikiana kwa karibu na wanajeshi wa DRC kupambana na kundi na ADF washirika wake wanaoendeleza shuguli zake nchini DRC.
Uganda imetuhumiwa na wataalam wa Umoja wa Mataifa kuwaunga waasi wa M23 mkono kwa kutumia ardhi yake katika shughuli zao wa usafiri, madai ambayo Uganda imekanusha.