Shirika la Utangazaji la Ujerumani - DW limeapa kuchukua hatua ya kisheria baada ya Urusi kulipiga marufuku kuendesha shughuli zake nchini humo. Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Urusi imetangaza jana kuwa ofisi za DW mjini Moscow zifungwe na kuvifuta vibali vya kazi vya waandishi wa habari wa shirika hilo. Mkurugenzi Mkuu wa DW Peter Limbourg amelaani hatua hiyo akiapa kuwa shirika hilo la utangazaji litaendelea kuripoti kuhusu matukio ya Urusi bila kuzuiwa. Hatua ya Moscow ilichukuliwa haraka kulipiza kisasi uamuzi wa Jumatano wa Tume ya utoaji Leseni na Usimamizi - ZAK, shirika linalosimamia vyombo vya habari Ujerumani, kuipiga marufuku televisheni ya RT DE inayomilikiwa na serikali ya Urusi kutangaza nchini humo kutokana na kutokuwa na leseni. Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ujerumani imelalamikia hatua hiyo ikisema itaharibu hata zaidi mahusiano kati ya nchi hizi mbili. DW, imekuwa na leseni ya utangazaji nchini Urusi tangu mwaka wa 2005.