Mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda Alhamisi Februari 27, 2025 ameipa mwezi mmoja Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa TAKUKURU mkoa wa Arusha kuhakikisha wanafanya uchunguzi, kuwahoji na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wahusika wote wanaodaiwa kuiba takribani Milioni 400 zilizokuwa mali ya Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa imekuja kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Viongozi wa Umoja huo wa bodaboda kwenye Kikao maalum cha kamati ya ushauri ya mkoa, kilichoketi leo kujadili makadirio ya mpango wa bajeti ya mwaka 2025/2026 ambapo inadaiwa kuwa mwaka 2018, wadau mbalimbali walichangisha fedha hizo na kuwekwa kwenye akaunti maalum ya umoja huo na baadae kuanza kuchotwa kupitia matawi mbalimbali ya benki na waliokuwa Viongozi wa Umoja huo.
Wakati wa kikao hicho, Katibu wa Umoja huo mkoa wa Arusha Hakim Msemo mbeke ya Wajumbe wa RCC amehoji ni kwanini imekuwa ngumu kwa watuhumiwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani licha ya kuwa yeye binafsi amewahi kusafiri mpaka Dar Es salaam na kupata taarifa za wahusika na kisha kuzifikisha TAKUKURU lakini bado kumekuwa na kigugumizi katika kuwachukulia hatua.
Makonda katika maelezo yake ameeleza kulifahamu suala hilo kabla hata hajawa Mkuu wa Mkoa, akitoa hadi Machi 27, 2025 TAKUKURU itoe ripoti kwa wanahabari kuhusu uchunguzi wa suala hilo na ikiwa hakutokuwa na majibu Mkoa utahitimisha kuwa baadhi ya maafisa wa TAKUKURU nao ni miongoni mwa wanufaika wa wizi huo.