Vatican inasema kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis anaendelea vyema hospitalini kwa siku ya pili mfulilizo.
Baada ya kulazwa katika hospitali ya Gemelli mjini Rome tarehe 14 ya mwezi Februari kutokana na matatizo ya kupumua, hali ya kiafya ya Papa ilizua wasiwasi baada ya homa ya mapafu kusambaa kwenye mapafu yake mawili.
Licha ya wasiwasi hiyo, taarifa ya Vatican imeonekana kurejesha matumaini kwa wafuasi wa Kanisa Katoliki duniani.
Baada yake kukabiliwa na wakati mgumu wikendi iliopita, Vatican wiki hii imekuwa ikitoa taarifa ikisema kwamba Papa Francis ambaye amekuwa kiongozi wa kanisa Katoliki tangu mwaka wa 2013 anaendelea kupata nafuu.
Wataalam wa afya kwa upande wao wameonya kwamba huenda Papa akachukua muda zaidi kupona kutokana na umri wake mkubwa na kiwango cha homa ya mapafu anachokabiliwa nacho.
Papa ameendelea kufanya kazi akiwa hospitalini ambapo anapata nafuu na kufanya maombi akiendelea pia kuangaliwa na madaktari kwa mujibu wa taarifa ya Vatican.
Hii ni mara ya nne kwa papa kulazwa hospitalini katika kipindi cha miaka 12 ya uongozi wake, mara hii akilazwa kwa muda mrefu zaidi.Awali kiongozi huyo anatumia kiti cha magurudumu kutembea kutokana na changamoto kwenye goti lake na paja.