ICC imetoa wito kwa makundi ya waasi kuheshimu sheria za kimataifa

Mwendesha mashtaka Mkuu katika Mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu ICC, Karim Khan ametoa wito kwa makundi yote yenye silaha mashariki ya DRC kuheshimu sheria za kimataifa.


Wito wa Khan unakuja wakati huu mapigano yakionekana kusambaa katika maeneo mbalimbali ya mashariki ya taifa hilo.

Khan aliwasili jijini Kinshasa siku ya Jumatatu ya wiki hii katika ziara anayosema itahusisha mikutano mbalimbali akitarajiwa kukutana na rais Felix Tshisekedi na maofisa wengine wa serikali.

Siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu wa DRC Judith Suminwa akizungumza katika mkutano wa baraza kuu la haki za binadamu mjini Geneva alisema watu Elfu saba wameuawa tangu mwanzoni mwa mwezi Januari katika vita vya M23.

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa ICC imekuwa ikichunguza madai ya uhalifu dhidi ya binadamu uliotekelezwa tangu mwezi Julai mwaka wa 2002 katika eneo la Ituri pamoja na majimbo ya Kivu Kusini na Kaskazini tangu mwaka wa 2004.

Hadi kufikia sasa, mahakama ya ICC imewahukumu viongozi watatu wa makundi ya waasi nchini DRC kwa kuhusika kwao katika uhalifu dhidi ya binadamu mashariki ya taifa hilo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii