Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Joseph Kabila amesema kuwa, uongozi mbaya wa mrithi wake, Rais Felix Tshisekedi umechangia pakubwa kuzidisha mzozo mashariki mwa nchi hiyo.
Kabila amesema hayo katika makala yake kwenye gazeti la Afrika Kusini la Sunday Times na kuongeza kuwa, tangu Tshisekedi aingie madarakani mwaka wa 2019 baada ya kushinda uchaguzi wa 2018, hali nchini DRC imezidi kuzorota hadi kufikia kwenye hatua ya mpasuko.
Uchaguzi wa Disemba 2023 ambao ulimpa Tshisekedi muhula wa pili kwa kishindo ulikuwa wenye udanganyifu, alisema, akiishtumu serikali kwa kukandamiza upinzani wa kisiasa na rais kuwa dikteta.
“Vitisho, watu kukamatwa kinyume cha sheria, mauaji ya kiholela, pamoja na kutimuliwa kwa wanasiasa, waandishi wa habari na viongozi wa mashirika ya kiraia, wakiwemo viongozi wa makanisa, ni miongoni mwa sifa za utawala wa Tshisekedi,” alisema.
Wapiganaji wa M23 waliteka maeneo kadhaa kwa haraka katika wiki zilizopita na hadi sasa wanadhibiti maeneo makubwa ya mashariki mwa DRC yenye utajiri wa rasilimali, huku kukiwa na hofu kwamba mzozo huo unaweza kuvuka mipaka.
Wakati huo huo, Tanzania leo Jumatatu, ni mwenyeji wa mkutano wa kikanda, kufuatilia matukio ya nyanjani DRC ili kuchukua hatua zinazohitajika za kukabiliana na mgogoro huo.
Mkutano huu unafanyika siku mbili baada ya viongozi wa majeshi ya Afrika Mashariki kukutana mjini Nairobi na kutoa mapendekezo ya kukabiliana na mzozo wa DRC.