Kulingana na msemaji wa jeshi la Israeli, Ariel na Kfir Bibas walikufa wakiwa kizuizini huko Gaza, " ambao waliuawa na magaidi wa Kipalestina mnamo Novemba 2023." Usiku wa Alhamisi tarehe 20 kuamkia Ijumaa Februari 21, serikali ya Israeli pia imeishtmu Hamas kwa kukabidhi mwili wa mtu asiyejulikana badala ya mama wa watoto hao wawili, Shiri Bibas.
Wakati Hamas imekuwa ikidai mara kwa mara kwamba Ariel na Kfir Bibas - wenye umri wa miaka minne na miezi minane na nusu mtawalia walipotekwa nyara - waliuawa katika mashambulizi ya mabomu ya Israeli huko Gaza, msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee amesema kwenye Telegram usiku wa Alhamisi 20 kuamkia Ijumaa Februari 21 kwamba watoto hao wawili "waliuawa kikatili wakiwa kizuizini mnamo mwezi wa Novemba na magaidi wa Kipalestina ", " kulingana na tathmini ya mamlaka husika na kwa kuzingatia viashiria vya kijasusi na uchunguzi vinavyopatikana".
Kfir Bibas alikuwa mtoto wa mwisho kati ya mateka 251 waliotekwa nyara mnamo Oktoba 7, 2023. Baba mwenye umri wa miaka 35 wa watoto hao wawili aliachiliwa mnamo Februari 1.
Katika mchakato huo, Avichay Adraee alitoa shutuma ya pili dhidi ya Hamas, akisema kwamba moja ya miili minne kundi hilo lililokabidhi kwa taifa la Israeli siku ya Alhamisi, Februari 20, haikuwa ya mama wa watoto hao wawili, Shiri Bibas, wala kwa hakika "mwili wa mateka yeyote wa Israeli." "Hiki ni huu ni mwili wa mtu asiyejulikana," msemaji huyo wa kijeshi amesema, akilaani "ukiukaji wa wazi" wa makubaliano ya kusitisha mapigano. "Tunaitaka Hamas iwarejeshe Shiri Biba na wote waliotekwa nyara," amesema.
Mwili wa nne uliorejeshwa Israeli siku ya Alhamisi ni ule wa Oded Lifshitz, mwandishi wa habari wa zamani ambaye alikuwa na umri wa miaka 83 siku ya kukamatwa kwake, Oktoba 7, 2023.
Miili hiyo minne ilikabidhiwa saa chache mapema na Hamas kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) na kisha kwa jeshi la Israeli, ikiwa ni sehemu ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza ambayo yalianza kutekelezwa Januari 19 na ambayo tayari yameruhusu kuachiliwa kwa mateka 19 wa Israeli badala ya zaidi ya Wapalestina 1,100 wanaoshikiliwa katika jela za Israeli.
Kabla ya Israeli kuishutumu Hamas kwa kukabidhi maiti ambayo haijatambuliwa badala ya Bibi Bibas, maelfu ya watu walisimama katika uwanja wa mateka wa Tel Aviv, wakiinamisga vichwa vyao chini, macho yakiwa yamefunikwa, mikono ikiwa imeshikana au kushikilia mabango, wakikaa kimya kwa dakika moja wakati wa mkesha wa kuwasha mishumaa kwa kuwakumbuka mateka waliofariki.
Hii ni mara ya kwanza kwa Hamas kukabidhi miili ya mateka tangu shambulio la Oktoba 7, 2023 katika ardhi ya Israel. Jeshi la Israel pia lilipata miili kadhaa ya mateka wakati wa operesheni zake huko Gaza.