Mbunge wa Bunda Vijijini, Mwita Getere ameibua tena sakata la wabunge kudai mikataba ya miradi mikubwa ipelekwe bungeni ili waipitie.
Katika swali la msingi mbunge huyo ameitaja mikataba ya miradi ya madini, ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere na Bomba la gesi ya Mtwara - Dar es Salaam.
Katika maswali hayo ambayo yaliulizwa leo Ijumaa Februari 4, 2022 na Cecil Mwambe kwa niaba yake, mbunge huyo amehoji pia iwapo miradi hiyo inakaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katika swali la nyongeza, Mwambe ameomba majibu ya lini mikataba hiyo na mikataba mingine ambayo inatiliwa shaka itapekwa bungeni badala ya majibu kuwa ukaguzi wake hupitia kamati za bunge.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Katiba Geofrey Pinda amesema kuwa mikataba hiyo inafanyiwa ukaguzi unaotakiwa kupitia kamati za bunge.
Hata hivyo Pinda amesema mikataba hiyo inaweza kupelekwa bungeni ikiwa itahitajika kwa kufuata kanuni za kibunge kwani haina shida yoyote.