Wizara ya ulinzi ya Marekani imesema inao ushahidi kuhusu mpango wa Urusi kutoa mkanda bandia wa video, ikionyesha kitakachoelezwa kuwa ni shambulizi la Ukraine, ili iutumie kama kisingizio kuivamia nchi hiyo.
Msemaji wa wizara hiyo, John Kirby amewaambia waandishi wa habari mjini Washington, kuwa kisingizio hicho cha Urusi kitadai kuwa jeshi la Ukraine au kikosi chake cha ujasisi kimefanya shambulizi dhidi ya Urusi yenyewe, au dhidi ya watu wanaozungumza lugha ya Kirusi.
Kulingana na msemaji huyo wa wizara ya ulinzi ya Marekani, mkanda huo wa vidio wa Urusi utaonyesha maiti za wahanga wa shambulio hilo na waombolezaji na picha za miundombinu iliyoharibiwa, na kudai kuwa shambulizi limefanywa kwa kutumia silaha ambazo Ukraine imezipata kutoka nchi za magharibi.
Mara zote Urusi imekuwa ikikanusha tuhuma za nchi za magharibi kuwa ina azma ya kuivamia Ukraine