Bobi Wine amjibu Mkuu wa majeshi Uganda kwa kutishiwa kukatwa kichwa

Vita vya mitandaoni vimeendelea kutokota kati ya Mkuu wa jeshi la Uganda Generali Muhoozi Kainerugaba na mwanasiasa mashuhuri wa Uganda Bobi Wine.

Hii ni baada ya mtoto wa Rais wa muda mrefu Yoweri Museveni, kusema kuwa anataka kumkata kichwa kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo Bobi Wine.

Katika chapisho kwenye X Jumapili jioni, Kainerugaba alisema babake aliyeitawala Uganda tangu 1986, ndiye mtu pekee anayemlinda kiongozi wa upinzani Bobi Wine dhidi yake.


Bobi wine ambaye aliibuka wa pili katika uchaguzi wa urais 2021 ulioshindwa na Yoweri Museveni, amejibu vitisho vya mtoto wa rais akisema kuwa kauli hizo anazichukulia kwa uzito kutokana na vitisho vya kuuawa.

Naye Kainerugaba ambaye ni mtoto wa rais akamjibu: “Nimekuamsha? Kabla nikumalize kwanza tulipe mkopo tuliokupa,” akionekana kudai kuwa serikali ilikuwa imelipa Bobi Wine apunguze joto la upinzani nchini humo.

Hata hivyo msemaji wa serikali ya Uganda pamoja na Kainerugaba hawakupatikana kuzungumzia kauli hizi za mitandaoni.

Naye msemaji wa wanajeshi nchini Uganda alikataa kuzungumzia mtafaruku uliopo.

Awali msemaji wa serikali alisema kauli za Kainerugaba mitandaoni zinapaswa kuchukuliwa kama “stihizai” na hazipaswi kuchukuliwa kwa uzito au kupima sera za serikali ya Uganda.

Bobi Wine amepinga vikali madai kuwa alihongwa na serikali ya Uganda katika shughuli zake za kuwania urais mwaka 2021. “Iwapo walinifadhili kwanini wananifuata kila mahali na kuua wafuasi wangu?” Bobi Wine anasema.

Bobi wine ambaye jinalake halisi ni Robert Kyagulanyi alikuwa mwanamiziki na kugeukia siasa amekuwa kigogo wa kupinga utawala wa rais Yoweri Museveni.

Katika chaguzi za 2021 Bobi Wine alipinga matokeo ya uchaguzi akidai uchaguzi uliingia dosari kwa wizi na wapiga kura kutishiwa maisha.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii