WASICHANA watatu katika Kaunti ya Narok wanaendelea kufanya mitihani ya kitaifa ya sekondari (KCSE) wakiwa hospitalini baada ya kujifungua saa chache kabla ya kuanza kwa mtihani Jumatatu.
Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Narok Apolo Apuko alithibitisha kwamba wasichana hao ni wa Shule ya Sekondari ya St. Antony katika Kaunti Ndogo ya Narok Mashariki, Namnyak Girls iliyoko Narok Magharibi na Shule ya Sekondari ya Chepkoiyet katika Kaunti Ndogo ya Trans Mara Mashariki.
Bw Apuko alisema wasichana hao wako katika hali nzuri ya kiafya na wanafanya mitihani yao chini ya uangalizi mkali, kama wenzao shuleni.
Vile vile, Bw Apuko alitoa wito kwa wananchi kuwapa watahiniwa msaada wanaohitaji katika msimu wa mtihani wa kitaifa.
“Jukumu letu kama wadau wa elimu ni kuhakikisha mtihani unafanyika katika mazingira mazuri na watoto wanafanya mtihani ufaao kwa wakati ufaao. Tunawaomba wananchi wote watuunge mkono kwa kujiepusha na eneo la shule,” aliomba.
Kulinga na afisa huyu wa elimu, takriban watahiniwa 17, 300 wanafanya mtihani wa KCSE mwaka huu katika eneo hilo.
Kati yao, 9, 500 ni watahiniwa wavulana huku wasichana wakiwa 7,800.
Watahiniwa hao wanafanya mitihani hiyo katika vituo 196 katika kaunti ya Narok.
Akizungumza wakati wa kufunguliwa kwa shehena ya mtihani katika afisi ya Kamishna wa Kaunti ya Narok mnamo Jumatatu, Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) Dkt David Njengere aliwarai watahiniwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kujiepusha na matatizo.