Hali ya utulivu imeonekana kurejea katika mji mkuu wa Guinea-Bissau,
wakati serikali ikianzisha uchunguzi wa kile ilichokitaja kuwa jaribio
la mapinduzi lilolenga kumwondoa madarakani rais Umaro Sissoco Embalo.
Rais huyo alinusurika shambulio la risasi siku ya Jumanne huku maafisa
11 wakiuwawa, kulingana na taarifa ya serikali. Washambuliaji
waliojihami kwa silaha walivamia majengo ya serikali katika mji mkuu wa
Bissau ambako rais Embalo alikuwa akiendesha kikao cha baraza la
mawaziri. Baadae rais huyo aliwaeleza waandishi wa habari kwamba yuko
salama na hakudhurika wakati wa majibizano ya risasi yaliyodumu kwa
karibu saa tano. Ameliezea shambulio hilo kuwa njama ya kutaka
kuiangusha serikali nzima. Jumuiya ya kikanda ECOWAS na Umoja wa Afrika
umeelezea wasiwasi mkubwa juu ya jaribio hilo la mapinduzi.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii