Jirani Aliyemchoma Mtoto Moto Kisa Chenji Adakwa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Juma Afyusisye (38), Dereva Bodaboda, Mkazi wa Iwambi Jijini Mbeya kwa tuhuma za kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili Mwanafunzi wa kiume wa darasa la pili wa Shule ya Msingi Iwambi Mkazi wa Iwambi kwa kumchoma moto.


Taarifa iliyotolewa leo November 09,2024 na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, imesema “Ni kwamba mnamo November 05, 2024 maeneo ya Iwambi Jijini Mbeya, Juma Afyusisye (38), Dereva Bodaboda, Mkazi wa Iwambi alimpatia fedha kiasi cha Tsh.10,000, Mhanga (Mtoto wa Jirani yake) na kumuagiza aende dukani kumnunulia maandazi ya Tsh. 5,000 lakini Mhanga aliitumia pesa yote kwa matumizi yake binafsi”


“Mhanga baada ya kurudi na kuonekana hana pesa ndipo Mtuhumiwa Juma Afyusisye alijichukulia sheria mkononi kwa kummwagia mafuta ya petroli kwenye shati alilovaa na kisha kuwasha kiberiti na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake, Mhanga amelazwa Hospitali Teule – Ifisi katika Mji mdogo wa Mbalizi akiendelea kupatiwa matibabu”


“Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wazazi/Walezi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watafute njia sahihi ya kuwaadhibu Watoto pindi wanapokosea, Jeshi la Polisi linaendelea kusisitiza kuwa halitavumilia wala kufumbia macho vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika jamii, litaendelea kuchukua hatua kali kwa Watuhumiwa kwa mujibu wa sheria”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii