Kiwanda cha nguo chateketea kwa moto huku 16 wafariki dunia

Takriban watu 16 wamefariki dunia baada ya moto mkubwa kuzuka katika kiwanda cha nguo nchini Bangladesh, huku maafisa wakisema kuwa huwenda idadi hiyo ikaongezeka.

Shirika la zimamoto limesema miili 16 imepatikana lakini iliungua kiasi cha kutotambulika.

Ndugu na jamaa wakiwa katika hali ya wasiwasi walikusanyika nje ya kiwanda cha ghorofa nne katika eneo la Mirpur huko Dhaka, kuwatafuta wapendwa wao ambao bado hawajapatikana.

Serikali imesema moto huo uliozuka katika kiwanda hicho majira ya saa sita mchana, ulizimwa baada ya saa tatu, lakini ghala la kemikali lililo karibu liliendelea kuwaka.

Mkurugenzi wa Huduma ya Zimamoto Mohammad Tajul Islam Chowdhury aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa waathiriwa walikufa papo hapo baada ya kuvuta gesi yenye sumu kali.

Pia Bw. Chowdhury aliongeza kusema polisi na maafisa wa kijeshi bado wanajaribu kuwatafuta wamiliki wa kiwanda na ghala hilo na uchunguzi kuhusu iwapo ghala hilo lilikuwa likifanya kazi kihalali pia unaendelea.

Wanafamilia waliokuwa na machozi walisimama nje ya majengo yaliyokuwa yameungua wengi wao wakiwa wameshikilia picha za jamaa zao waliopotea.

Miongoni mwao ni mwanaume anayemtafuta binti yake, Farzana Akhter.

"Niliposikia kuhusu moto, nilikuja mbio. Lakini bado sijampata....namtaka binti yangu," aliliambia Shirika la Habari la Reuters.

Mwaka 2021 moto katika kiwanda cha chakula na vinywaji uliwaacha watu wasiopungua 52 wakiwa wamefariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa. Kiwanda hicho kilijengwa kinyume cha sheria na hakikuwa na mlango wa dharura, uchunguzi ulieleza.

Ajali mbaya zaidi ya viwanda nchini humo hadi sasa ilitokea mwaka 2013, wakati jengo la biashara la ghorofa nane liliporomoka na kuua zaidi ya watu 1,100.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii