Watu 300,000 walitoroka Sudan Kusini mnamo mwaka 2025 kufuatia mgogoro wa kivita

Takriban watu 300,000 wameikimbia Sudan Kusini tangu mwanzoni mwa mwaka 2025, huku mzozo kati ya viongozi wanaohasimiana ukitishia kuzua vita vya wenyewe kwa wenyewe, Umoja wa Mataifa unaonya.

Kutoroka kwa watu hawa wengi kuliripotiwa siku ya Jumatatu na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu nchini Sudan Kusini. Ripoti hiyo inaonya juu ya hatari ya kurejea kwa vita kamili vinavyohusishwa na mzozo kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wa Kwanza wa Rais aliyesimamishwa kazi Riek Machar.

Ripoti ya tume hiyo inataka uingiliaji wa haraka wa nchi za kikanda ili kuzuia nchi kuingia katika janga kama hilo.

Sudan Kusini imekuwa ikikumbwa na misukosuko ya kisiasa na ghasia za kikabila tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011.

Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka wa 2013 wakati Kiir alipomfukuza Machar kama makamu wa rais. Wawili haao walifikia makubaliano ya kusitisha mapigano mwaka wa 2017, lakini makubaliano yao tete ya kugawana madaraka yamekuwa yakumbwa na vurugu kwa miezi kadhaa na yalisitishwa mwezi uliopita kufuatia kuzuka kwa ghasia kati ya vikosi vinavyotii kila mmoja kati ya wawili hao.

Machar aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani mwezi Machi baada ya mapigano kati ya jeshi na wanamgambo wa Nuer katika mji wa kaskazini mashariki wa Nasir yaliyogharimu maisha ya watu kadhaa na wengine zaidi ya 80,000 kuwa wakimbizi.

Alishtakiwa kwa uhaini, mauaji, na uhalifu dhidi ya ubinadamu mwezi Septemba, ingawa wakili wake alidai mahakama hiyo haina uwezo wa kushughulikia kesi hiyo. Kiir alimsimamisha kazi Machar mapema mwezi Oktoba.

Machar anakanusha tuhuma hizo, huku msemaji wake akisema ni "kesi ya kisiasa."

Kuongezeka kwa mapigano nchini Sudan Kusini kumesababisha karibu watu 150,000 kuingia Sudan, ambako vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili vimepamba moto, na idadi sawa na hiyo katika nchi jirani ya UgandaEthiopia, na Kenya.

Zaidi ya wakimbizi milioni 2.5 wa Sudan Kusini sasa wanaishi katika nchi jirani, huku milioni mbili wakisalia kuwa wakimbizi wa ndani.

Tume imehusisha mgogoro wa sasa na ufisadi na ukosefu wa uwajibikaji miongoni mwa viongozi wa Sudan Kusini.

"Mgogoro wa sasa wa kisiasa, kuimarika kwa mapigano, na ufisadi wa kimfumo na usiodhibitiwa ni dalili za kushindwa kwa uongozi," amesema Kamishna Barney Afako.

"Mgogoro huo ni matokeo ya uchaguzi wa makusudi wa viongozi wake kuweka masilahi yao wenyewe kabla ya yale ya watu wao," Mwenyekiti wa Tume Yasmin Sooka amesema.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa mwezi Septemba ilifichua ufisadi mkubwa, ikidai kuwa dola bilioni 1.7 kutoka kwa mpango wa "mafuta kwa barabara" bado hazijulikani zilipo, wakati robo tatu ya nchi inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Kamishna Barney Afako ameonya kwamba bila ushiriki wa mara moja wa kikanda, Sudan Kusini inaweza kukabiliwa na hali nzito.

"Wasudan Kusini wanategemea Umoja wa Afrika na kanda kuwaokoa kutokana na hatima inayoweza kuepukika," amesema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii