Vikosi maalum vya Marekani vimefanya uvamizi dhidi ya ugaidi katika eneo linaloshikiliwa na upinzani kaskazini-magharibi mwa Syria, karibu na mpaka wa Uturuki, Pentagon imesema.
Msemaji alisema kuwa ujumbe huo ulifanikiwa na kwamba hakuna majeruhi wa Marekani, lakini hakutoa maelezo mengine.
Huduma ya uokoaji ya Helmet Nyeupe iliripoti kuwa takriban watu 13, wakiwemo watoto sita na wanawake wanne, waliuawa katika mji wa Atmeh.
Eneo hilo linaaminika kuwa makazi ya wanajihadi wa kigeni wanaohusishwa na al-Qaeda.
Wakazi wa Atmeh walisema helikopta kadhaa zilitua hapo karibu usiku wa manane siku ya Alhamisi (22:00 GMT siku ya Jumatano) na kwamba walisikia milio ya risasi kwa saa mbili.
Shirika la kutete Haki za Kibinadamu la Syria Observatory, kundi la waangalizi lenye makao yake makuu nchini Uingereza, limesema operesheni hiyo ya Marekani ni kubwa zaidi kaskazini-magharibi mwa Syria tangu kiongozi wa Islamic State (IS) Abu Bakr al-Baghdadi kufariki katika uvamizi wa kikosi maalum mwezi Oktoba 2019.