Maandamano ya CHADEMA yapigwa marufuku

Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano yaliyotangazwa na Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, yaliyotangazwa kufanyika Septemba 23, 2024 na kutia onyo kuwa yeyote atakayeingia barabarani atakabiliwa kwa mujibu wa sheria.

Akiongea hii leo Septemba 13, 2024 Msemaji wa Jeshi hilo Nchini Naibu Kamishna wa Polisi David Misime amesema September 11,2024 kupitia Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii walisikika Viongozi wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho akiwahamasisha Wakazi wa Dar es salaam kuingia barabarani kuanzia September 23,2024.

Amesema, “Viongozi hao waliendelea kuhamasisha Wananchi wa Kanda mbalimbali Nchini kukutana Dar es salaam ili kuungana na Wakazi wa Dar es salaam kuingia barabarani.”

Misime ameongeza kuwa, “hatua hiyo waliyofikia tunajiuliza na tunaendelea kufuatilia na kuchunguza kwanini wanataka kututoa kwenye reli ya hatua za kiupelelezi zinazoendelea baada ya Rais Samia kuviagiza Vyombo vya Uchunguzi vifanye uchunguzi kisha wawasilishe uchunguzi kwake”

Aidha, amesema mara kadhaa Viongozi na Wafuasi wa Chama hicho, wamekuwa wakipanga, kuratibu mikakati mbalimbali na kutoa matamshi yenye lengo la kuleta vurugu Nchini, ili kuharibu amani kwasababu wanazozijua.

“Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa Viongozi wa Chama hicho kuacha kuendelea kuhamasisha Wananchi kujihusisha katika uhalifu huo na yoyote atakayeingia barabarani atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria za Nchi,” alisisistiza DCP Misime.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii