Godbless Lema Afichua Jambo la Mbowe Kutaka Kuachia Nafasi ya Uongozi Chadema
Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amefichua taarifa za kushangaza kuhusu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Januari 14, Lema amesema Mbowe amemueleza mara kadhaa kuhusu dhamira yake ya kuachia nafasi ya uongozi wa chama hicho.
Kwa mujibu wa Lema, Mbowe alimwambia: “Bro, nataka kuachia chama hiki, jipangeni, nimechoka. Naapa Mungu ni shahidi haya maneno.
Kama nimesema uongo, wazazi wangu wafe na watoto wangu.
Lema amedai kuwa kauli hii ameisikia kutoka kwa Mbowe zaidi ya mara tano, akisisitiza kwamba Mwenyekiti huyo amekuwa na mawazo ya kustaafu uongozi wa chama.
Lema pia alifichua kuwa alipomuuliza Mbowe ikiwa ameandaa mrithi, Mwenyekiti huyo alijibu kuwa ndani ya mchakato wa kidemokrasia, hakuna kupanga mrithi.
“Kwenye democratic process huwezi kupanga successor, watu wanaibuka, wapiga kura wanaamua,” Lema alinukuu maneno ya Mbowe.
Katika mazungumzo hayo, Lema aliongeza kuwa hivi sasa kiongozi mwingine wa chama, Tundu Lissu, ameibuka kama mmoja wa wagombea wanaoweza kuchukua nafasi hiyo.
Kauli hizi zimeibua maswali mengi kuhusu mustakabali wa uongozi wa CHADEMA na hatma ya Mbowe, ambaye amekuwa mstari wa mbele kwa miaka mingi katika harakati za siasa za upinzani nchini Tanzania.
Taarifa hizi za Lema zimezusha mjadala mkali katika medani ya siasa, huku wadadisi wakitafakari iwapo ni ishara ya mabadiliko makubwa yanayokuja ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Wakati Mbowe hajatoa tamko rasmi, taarifa hizi bila shaka zitaendelea kuibua hisia tofauti ndani na nje ya CHADEMA.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii