Uchaguzi wa wabunge Comoro

Nchini Comoro, matokeo ya muda ya uchaguzi wa wabunge yamechapishwa jana, Jumanne Januari 14 jioni na Tume Huru ya taifa ya Uchaguzi baada ya kuchelewa kwa zaidi ya saa tatu kwa muda uliopangwa. Hali ambayo ilisababisha baadhi ya waangalizi, hasa wale kutoka Umoja wa Afrika, kuondoka kwenye chumba kabla ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa. Matokeo haya yaliyoonyesha ushindi mkubwa kwa chama tawala, yamezua hisia tofauti.

Kati ya viti 33 vitakavyojazwa, chama tawala cha CRC kimeshinda viti 28 katika duru ya kwanza ya uchaguzi. Wapinzani watatu pia tayari wamechaguliwa, huku majimbo mawili, Itsandra Sud na Nyumakele 3, yatalazimika kuamua kati ya wagombea wao wakati wa duru ya pili ya uchaguzi iliyopangwa Februari 16, siku ambayo uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika.

Mahamoud Fakridine, waziri anayehusika na uchaguzi, amekaribisha chaguo la raia na akapuuzia mbali ukosoaji wa upinzani: "Ninaamini kwamba watu wameamua. Sisemi kwamba kila kitu kilikuwa kamili, lakini nadhani kulikuwa na ukosoaji usiofaa katika baadhi ya ukweli. Kwa bahati mbaya pia ni njia ya wao kujitetea kuliko kusema kwamba hatukuwa na uwezo wa kuwashinda wagombea wa serikali, wanapendelea kusema kulikuwa na udanganyifu. Pia ni njia ya kujitetea. "

Upinzani au wakosoaji wana haki ya kukata rufaa hadi Ijumaa

Muungano wa Upinzani wa Comoro unaendelea kudai kuwa mchakato huo umekumbwa na kasoro. Uliamua kujiondoa katika mchakato wa uchaguzi. Wakili Fahmi Saïd Ibrahim El Maceli, mbunge wa zamani na sasa mgombea binafsi, amefuzu kwa duru ya pili. Pia anakemea hitilafu, lakini bado yuko kwenye kinyang'anyiro: "Ningependa tu kueleza kuwa mimi ni mgombea binafsi kwa hivyo sikuwa sehemu ya chama cha siasa. Kulikuwa na dosari nyingi, hasa kwa vile wakuu na makatibu wa vituo vya kupigia kura walichaguliwa kutoka ndani ya chama tawala. Kwa uchaguzi ujao, tutaomba uwazi na dhamana muhimu ili uchaguzi ufanyike katika mazingira bora zaidi."

Tume ya uchaguzi imeahidi kuwaadhibu maafisa wa vituo vya kupigia kura waliokiuka kanuni. Wagombea wana hadi Ijumaa, Januari 17, kuwasilisha rufaa zao katika Mahakama ya Juu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii