Thomas Tuchel Apewa Muda Na England

Thomas Tuchel kocha wa zamani wa Chelsea ya England ametangazwa na FA ya nchi hiyo kuwa kocha wao mkuu baada ya Gareth Southgate kujiuzulu mwezi Julai 2024. Kikosi cha Three Lions ( Simba Watatu ) kipo chini ya uangalizi wa kocha wa muda Lee Carsley ambaye ataiongoza timu hiyo mpaka Disemba 31 2024.

Tuchel raia wa Ujerumani amesaini mkataba wa miezi kumi na nane na atasaidiwa na Antony Barry ambaye aleshawahi kufanya naye kazi Chelsea na Bayern Munich. Kwa pamoja Makocha hao wataanza majukumu yao mapya katika timu ya taifa ya England Januari 1, 2025.

Mjerumani huyo aliyewahi kushinda tuzo ya Kocha bora wa mwaka wa Ulaya na Dunia mwaka 2021 baada ya mafanikio aliyoyapata msimu wa 2020-2021. Alikiongoza kikosi cha The Blues kushinda makombe ya klabu bingwa Ulaya pamoja na ubingwa wa klabu bingwa Dunia mwaka 2021. Mkufunzi huyo anahistoria ya kushinda makombe akiwa na Borrusia Dortmund ya Ujerumani , PSG ya Ufaransa na Chelsea ya England.

Baada ya kujiuzulu kwa Gareth Southgate FA ya nchi ya nchi hiyo mabingwa wa kombe la Dunia mwaka 1966, ilianza mchakato wa kutafuta Kocha mpya ambapo majina mengi yalitajwa mpaka pale viongozi wa Shirikisho hilo la Soka lilipoona Tuchel ndiye anayefaa kuiongoza timu ya taifa lao. Mkufunzi huyo wa zamani wa timu Matajiri wa Jiji la Paris alisaini mkataba tangu Oktoba 8, 2024 kutangazwa kwake kumecheleweshwa sababu za kupisha timu ya taifa iliyokuwa inashiriki michezo ya ligi ya mataifa ya Ulaya.

Kocha huyo wa Dunia mwaka 2021 anakuwa kocha wa tatu asiye raia wa Uingereza kuiongoza timu ya taifa ya England baada ya Sven- Goran Eriksson na Muitaliano Fabio Capello.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii