Real Madrid ya Hispania imepania kumsajili mlinzi wa kati wa klabu ya Arsenal raia wa Ufaransa William Saliba ili kuimarisha safu yao ya ulinzi inayomtegemea zaidi Antoni Rudiger, Saliba anatizamwa kama mrithi sahihi wa Kepteni wao wa zamani Sergio Ramos.
William Saliba yupo kwenye listi ya Wachezaji wanaohitajika kwenye kikosi cha Real Madrid pindi dirisha kubwa la uhamisho la mwezi Juni litakapofunguliwa. Mabingwa hao Watetezi wa La Liga wameweka wazi nia yao ya kumnasa Mlinzi huyo wa zamani wa Saint-Etienne ya nchini Ufaransa.
Florentino Perez ameweka wazi juu ya mahitaji ya Mlinzi huyo wa Arsenal ambaye inaaminika ndiye beki bora wa kati kwa sasa Duniani. Tangu Waondoke kikosini Sergio Ramos na Rafael Varane Madrid imepitia wakati mgumu wa kupata walinzi wa kati wenye ubora mkubwa, beki huyo anaonekana ni Mchezaji sahihi wa kutatua changamoto hiyo.
Saliba raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 22, mkataba wake ndani ya Arsenal utafika ukomo wake Juni 2027. Ukitaja majina ya mabeki watatu bora kwa sasa Duniani huwezi kuliacha nje jina la beki huyo wa Washika Mitutu wa Jiji la London. Wachezaji bora huwa wanavutiwa zaidi kucheza kwenye vilabu vikubwa vya nchini Hispania Real Madrid na Barcelona hivyo huwa ni ngumu kwa mchezaji kukataa pindi anapohitajiwa na timu hizo.
Kocha wa The Gunners Mikael Arteta anafahamu nguvu ya ushawishi ambayo vilabu vya Hispania iliyo nayo kwa Wachezaji kwani huwa wanahakikishiwa kushinda makombe sambamba na tuzo ya Ballon d'or, hivyo anafahamu kazi waliyonayo kumshawishi mchezaji huyo kusalia kwenye timu hiyo inayotumia uwanja wa Emirates.
Nyota huyo anayesifika kwa matumizi makubwa ya akili na utulivu awapo uwanjani anaweza kuvutiwa na mpango wa kujiunga na mabingwa hao wa Ulaya mara 15, kutokana na uwepo wa Wachezaji wengi vijana kwenye kikosi cha Madrid ambao ni raia wa taifa Ufaransa Wachezaji kama Eduardo Camavinga, Aurelien Tchouamen,Ferran Mendy na Kylian Mbappe.