Wakati Jeshi la Polisi likieleza jinsi mkaguzi msaidizi wa polisi Grayson Mahembe alivyojinyonga akiwa mahabusu, hatua iliyoibua hisia na maswali kadhaa, baba mzazi wa marehemu Gaitan Mahembe, ameendelea kulitaka jeshi hilo kuweka wazi uchunguzi wa kifo cha mwanawe.
Mahembe alikuwa miongoni wa maofisa wa jeshi hilo wanaodaiwa kumnyang’anya Sh33.7 milioni mfanyabiashara wa madini Mussa Hamis, kisha kuutupa mwili wake vichakani huku katika kijiji cha Namgogoro mkoani Mtwara Januari 5, 2022.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime imesema kuwa Grayson Mahembe aligundulika kujinyonga Januari 22, 2022 akiwa mahabusu kutokana na tuhuma za kumnyang’anya fedha na kisha kumuua Mussa Hamis na kuutupa mwili wake.
“Baada ya kufanya tukio hilo la ukiukwaji wa viapo vyao, akiwa na wenzake, wakiwamo maofisa, wakaguzi na askari wengine, hawakutoa taarifa kwa viongozi wao kwa sababu walifahamu kuwa wamefanya hivyo kwa nia ovu, kwa tamaa zao na kinyume cha sheria za nchi,” ilisema taarifa ya Misime