Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amekihakikishia Chama cha Watoa Huduma za
Simu Tanzania (TAMNOA) kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri
ya biashara yatakayo iwezesha Sekta Binafsi kukua na kuchangia ukuaji wa
uchumi wa Taifa.
Mhe. Nchemba alisema hayo jijini Dodoma
alipokutana na kuzungumza na Chama cha Watoa Huduma wa Simu Tanzania
(TAMNOA), wakati kikiwasilisha Serikalini maoni yao kuhusu sera za kodi
ikiwa ni maandalizi ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.
“Sekta
binafsi ikinawiri na Serikali inanawiri! Kwa sababu sekta binafsi ndiyo
injini ya kuwezesha ukuaji wa uchumi wetu, kwa hiyo niwashukuru kwa
maoni mliyotoa yakiwemo ya kutoza kodi maeneo yenye kipato kikubwa na
kutoa msamaha wa kodi kwa wale wenye kipato kidogo ili kupunguza pengo
la walio nacho na wasio nacho”, alisema Dkt. Nchemba.
Dkt.
Nchemba alisema kuwa dira ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, ni kuona sekta binafsi inafanya kazi kwa
mafanikio makubwa, kwa kuwa ni injini ya kukua kwa uchumi wetu, chanzo
cha ajira kwa vijana lakini pia ni chanzo cha mapato kwa Serikali, hivyo
ikikua na mapato ya Serikali yatakua.
Alisema kama Wizara
imepokea maoni hayo na itasimamia utekelezaji wake ili kuangalia mianya
mipya ya kutoza kodi hususani kampuni kubwa duniani zinazofanya biashara
kwa njia ya kidijiti kwa kuweka sheria ili kodi hizo ziweze kutumika
kutoa huduma kwa wananchi.
Aliwaelekeza wataalamu wa Wizara hiyo
kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia
mapendekezo yaliyotolewa na wadau hao ili kuona namna bora ya kuyatumia
mapendekezo hayo.
Aidha, Waziri Nchemba alitoa wito kwa wadau
wengine ikiwemo Sekta binafsi nchini kuwasilisha mapendekezo na maoni
yao mapema kuelekea maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa
fedha 2022/2023 ili kuwa na sera za kikodi rafiki kwa ajili ya
kuharakisha maendeleo ya nchi.
Alisema kuwa maoni na mapendekezo
kutoka sekta binafsi ni muhimu katika kusaidia maboresho ya sera za
kiuchumi na sera za kikodi ili kujenga mazingira rafiki kwa sekta
binafsi nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye, alisema kuwa mawazo yaliyotolewa
na wadau ni mazuri na kuwa Serikali imeyachukua na yatafanyiwa kazi na
kuiomba Wizara ya Fedha kuchambua maoni hayo mapema na kuwashirikisha
wadau kuhusu maamuzi yatakayofikiwa.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Fedha na Mipango Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Jamal
Kassim Ali, alisema kuwa suala la kuangalia namna ya kuzitoza kodi
kampuni kubwa duniani zinazofanya biashara kwa njia ya mtandao ni muhimu
kwa kuwa yanakusanya fedha nyingi kutoka kwa wananchi lakini haziachi
chochote kwa ajili ya maendeleo yao.
Kwa upende wao Chama cha
Watoa Huduma za Simu Tanzania (TAMNOA) walisema kuwa mapendekezo
waliyoyatoa yakifanyiwa kazi na kuanza utekelezaji wake mapato ya
Serikali yataongezeka kutoka asilimia 61 hadi asilimia 64.9