Makundi yenye silaha yanayotaka kujitenga nchini Mali yamekiri kuuawa kwa wapiganaji wake saba baada ya ndege isiyo na rubani kushambulia magari yao mawili kaskazini mwa nchi hiyo siku ya Jumatatu, katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Jumanne.
Jeshi la Mali kwa upande wake limedai kuharibu siku hiyo "magari mawili, yaliyokuwa yamepakia vifaa vya kivita vya makundi ya kigaidi yenye silaha, takriban kilomita 80 kaskazini mwa mji wa Anéfis".
Siku ya Jumapili, kulingana na makundi yanayotaka kujitenga, afisa aliyechaguliwa wa eneo hilo na mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la eneo hilo, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yalisababisha vifo vya watu ishirini, wakiwemo watoto kadhaa, huko Tinzaouatène karibu na mpaka na Algeria, ambapo jeshi la Mali na washirika wake wa Urusi walipata pigo kubwa katika mashambulizi ya wapiganaji wanaotaka kujitenga na wanajihadi mwishoni mwa mwezi wa Julai.
Kulingana na jeshi, ambalo linadai "kuangamiza watu ishirini wenye silaha", siku ya Jumapili walilenga " magaidi".
Utawala wa kijeshi nchini Mali ulivunja uhusiano na mkoloni wa zamani, Ufaransa na washirika wake wa Ulaya mnamo 2022, kuanzisha uhusiano wa kijeshi na kisiasa na Moscow.
Makundi yenye silaha yanayotaka kujitenga yamepoteza udhibiti wa maeneo kadhaa ya kaskazini tangu mwaka wa 2023, baada ya mashambulizi ya jeshi la Mali ambayo yaliishia katika kutekwa kwa Kidal, ngome ya madai ya uhuru na suala kuu la uhuru wa jimbo hilo kuu.
Mashambulizi kaskazini mwa nchi hiyo yamesababisha madai mengi ya dhuluma dhidi ya raia yaliyofanywa na vikosi vya Mali na washirika wao wa Urusi tangu 2022, ambayo mamlaka ya Mali inakanusha.