Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
amesema Serikali inaboresha Mfumo wa Uwazi wa Kupima Utendaji Kazi wa
Taasisi unaojulikana kama Mfumo wa Mikataba ya Utendaji Kazi katika
ngazi ya Taasisi za Umma kuwa wa kielektroniki ili utumike kupima
utendaji kazi wa taasisi za umma nchini.
Akizungumza ofisini
kwake Jijini Dodoma, Mhe. Jenista amesema, mfumo huo wa kielektroniki
utawezesha makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi za
Umma kuhusu malengo ambayo Taasisi husika itayatekeleza katika kipindi
cha mwaka mmoja.
“Malengo yaliyomo ndani ya Mkataba yatakuwa na
vigezo, shabaha na viashiria vitakavyotumika kupima utendaji kazi wa
Taasisi kila mwisho wa mwaka. Mkataba huu unalenga kuimarisha dhana ya
utendaji unaojali matokeo, kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi,
na kuongeza uwajibikaji wa viongozi katika Taasisi za Umma,” Mhe.
Jenista amefafanua.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, Mfumo huo wa
kielektroniki ukikamilika utatumika kulinganisha na kushindanisha
utendaji wa taasisi na kutoa tuzo za utendaji bora kwa taasisi zenye
utendaji mzuri kila mwaka.
Akizungumzia faida za Mfumo huo, Mhe.
Jenista amesema utaongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa Sera,
Mikakati na Vipaumbele vya Taasisi, Sekta na Taifa kwa ujumla ikiwa ni
pamoja na kuboresha utoaji huduma kwa umma, kuimarisha utamaduni wa
utendaji unaojali matokeo na kuleta matumizi bora ya rasilimali za Umma.
Aidha, Mhe. Jenista amewataka Makatibu Wakuu na Watendaji
Wakuu wote wa Taasisi za Umma kuendelea kusimamia utekelezaji wa mfumo
huu kikamilifu na wahakikishe wanatenga bajeti kwa ajili ya kusimamia
utekelezaji wake katika Taasisi wanazoziongoza.
Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imejipanga vizuri
kujenga na kusimamia mifumo yenye tija kupitia sekta ya Utumishi wa
Umma.