Ripoti yaelezea sababu za kuibuka tena kwa kundi la waasi la M23

Ripoti ya Ebuteli na kundi la Utafiti kuhusu Kongo (GEC) iliyochapishwa siku Jumanne, Agosti 6, 2024, yenye kichwa Kuibuka tena kwa M23: ushindani wa kikanda, siasa za wafadhili na kuzuia mchakato wa amani, inathibitisha kwamba sababu za kuzuka upya kwa waasi wa M23 ni ushindani wa kisiasa na Uganda. Na hii, kinyume na kile Rwanda, msaadizi mkuu wa waasi katika jimbo la Kivu Kaskazini, inadai.


Mnamo mwaka 2021, Kigali ilikuwa na hisia ya kutengwa katika kanda nzima na kuona maslahi yake yakitishiwa nchini DRC wakati Kinshasa ikianzisha uhusiano na Kampala kwa kusaini mikataba, hasa ya kiuchumi na usalama.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kigali ilikuwa na hisia ya kutengwa wakati timu za Uganda zilipoanza ujenzi wa barabara za kuunganisha mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri hadi Kampala, hali ambayo ilihatarisha kuiondoa Rwanda katika biashara ya faida kati ya Mashariki ya Kongo na pwani ya Afrika Mashariki.

Ripoti hiyo inapuuzilia mbali madai ya Rwanda: kuna ushahidi mdogo wa kuongezeka kwa ghasia dhidi ya Watutsi huko Kivu Kaskazini kabla ya kuzuka upya kwa M23. Kwa hiyo ilikuwa ni tarehe 7 Novemba 2021 ambapo M23, walioshindwa mwaka wa 2013, walianzisha mashambulizi upande wa kaskazini na magharibi mwa Mlima Sabinyo kwa ombi la Kigali. Udhaifu wa serikali ya Kongo ulizidisha mzozo huu. Serikali ya Kongo ilitumia makampuni binafsi ya ulinzi na ushirikiano na makundi ya kigeni na ya ndani yenye silaha ilik kukabiliana na mashambulizi ya waasi hao.

Hata hivyo, inabainisha ripoti, makundi haya - kama vile M23 - huajiri hasa kwa misingi ya kikabila, ambayo imezidisha mivutano ya kijamii na kikanda.

Kwa upande wa kidiplomasia, mwitikio wa kimataifa umekuwa duni, Kigali ikiwa bado haijakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi kama ilivyoombwa na Kinshasa.

Makundi hayo mawili ya utafiti yanapendekeza kwamba mamlaka ya Kongo irekebishe sekta ya usalama.

Vikosi vya kijeshi, "ambavyo vinatumika kwa kiasi kikubwa kusambaza haki na rasilimali", lazima vibadilishwe kuwa huduma halisi ya umma.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii