Dkt. Kijaji "Mauzo ya bidhaa soko la Ulaya yameongezeka"

Serikali Nchini, imesema thamani ya mauzo ya bidhaa za kwenda katika soko la Ulaya kwa mwaka 2023 iliongezeka hadi kufikia shilingi Trilioni 3.836, kutoka shilingi Trilioni 2.446 kwa mwaka 2022 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 56.8

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji ameyasema hayo hii leo Mei 21,2024 Bungeni Jijini Dodoma, wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na biashara na kudai kuwa ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa za kilimo na viwandani kwenda katika nchi hizo.

“Uagizaji wa bidhaa kutoka Jumuiya ya ulaya ulipungua kwa asilimia 8.1 hadi shilingi Trilioni 4.404 kwa mwaka 2022 huku sababu zikiwa ni pamoja na kupungua kwa mahitaji ya bidhaa za Viwandani na mitaji kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa zilizokuwa zinaagizwa
kutoka soko la ulaya ikiwemo vilainishi vya magari,” alisema.

Dkt. Kijaji amesema, kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutafuta fursa za uwekezaji biashara na soko nje ya nchi zimefungua milango na madirisha ya biashara kwa soko la ndani na nje na kuongeza kuwa sekta ya viwanda nchini imeendelea kukua na kufikia asilimia 4.3 mwaka 2023, ikilinganishwa na asilimia 4.2 mwaka 2022.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii