Mbunge ataka serikali isisimamie mwendokasi

Mbunge wa Jimbo la Kwimba mkoani Mwanza Mansoor Shanif Jamal, ameishauri serikali kutangaza tenda kwa Watanzania wenye uwezo wa kuendesha na kusimamia mradi wa mabasi ya mwendokasi ili wananchi wa Dar es Salaam wasiendelee kupata adha ya usafiri

Kauli hiyo ameitoa hii leo Juni 20, 2024, Bungeni jijini Dodoma, wakati akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024 / 2025.

"Serikali Hamuwezi mkajenga mradi mkauendesha wenyewe, hizo barabara za mwendokasi mlizozijenga ningewashauri mtangaze tenda, Watanzania ambao wana uwezo wa kuleta mabasi 50 na kuendelea yanayofanana na yale ya mwendokasi wawekeze waje watumie barabara zenu, mtu akitaka kupanda basi zake apande kama ni VIP atachaji pesa yake ili mradi huduma ipatikane," amesema Mbunge Mansoor Shanif Jamal

Aidha Mbunge huyo ameongeza kuwa, "Dar es Salaam yote imechafuka kwa sababu ya mwendokasi lakini mabasi hakuna na barabara ziko tupu mimi ningeshauri sana serikali isinunue mabasi, itoe kibali wafanyabiashara wa Kitanzania wapo wanunue mabasi 50 na kuendelea watumie zile barabara watoe huduma kwa wananchi,".


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii