Tabora United yawakuta mazito

Mchezaji kutoka DR Congo Makuntima Kisombe Guylain ameiwekea kigingi klabu ya Tabora United kufanya usajili, baada ya kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo ya mkoani Tabora.

Uamuzi wa kufungiwa kufanya usajili kwa klabu hiyo umetolewa na Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ baada ya kukaidi maagizo ya kulipwa kwa Guylain ndani ya siku 45, tangu uamuzi huo ulipotolewa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ imeeleza kuwa, FIFA imeifungia Tabora United kufanya uhamisho wa wachezaji Kimataifa, sambamba na uhamisho wa ndani.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF Cliford Mario Ndimbo imeeleza: Klabu ya Tabora United inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC, imefungiwa kufanya usajili mpaka itakapomlipa aliyekuwa mchezaji wake Makuntima Kisombe Guylain.

Uamuzi huo umefanywa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) baada ya mchezaji huyo kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo.

Guylain raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) alifungua kesi FIFA akidai malipo ya malimbikizo ya mishahara.

Klabu hiyo ilitakiwa iwe imemlipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini haikutekeleza hukumu hiyo.

Wakati FIFA imeifungia klabu hiyo kufanya uhamisho wa wachezaji kimataifa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) nalo limeifungia kufanya uhamisho wa ndani.

TFF inazikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo zimeingia na wachezaji pamoja na makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kusajili.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii