MWANAMUZIKI wa mtindo wa Africapopster Nadia Mukami amejitokeza kulaumu Chama cha Hakimiliki za Muziki Nchini (MCSK) kwa kukosa kumpa pesa zake tangu mwaka 2017.
Mwanamuziki huyo amelaumu uongozi wa Dkt Ezekiel Mutua katika MCSK akidai wanabagua wanamuziki nchini.
Aidha alidai kwamba maafisa wa MCSK wameshindwa kueleza jinsi walivyotumia Sh56 milioni zilizokusanywa kutokana na kazi za wasanii mwaka wa 2023.
Nadia alisema kuwa alijiandikisha rasmi kuwa mwanachama wa MCSK mwaka 2017 kama msanii mpya.
Ajabu ikiwa miaka saba sasa, licha ya ngoma zake kuvuma na kuwa maarufu ndani na nje ya nchi, hajawahi kupokea hata shilingi moja.
“Kweli mimi ni mwanachama. Nasikitika kufikia sasa sijawahi kupokea pesa zozote za MCSK. Mimi binafsi nimekuwa maarufu. Kabla nijiunge, nilianza kuwa maarufu na nikaona umuhimu wa kujiunga. Mbona mimi MCSK?” aliuliza Bi Mukami.
Msanii huyo hajawahi kupokea mapato yake kutokana na kazi zake ambazo zimeenea pakubwa hadi kujizolea tuzo ya AFRIMMA katika kategoria ya msanii bora wa kike ukanda wa Afrika Mashariki mwaka 2023.
Usimamizi wa MCSK umekuwa ukivuna sana na mwaka huu wamesambaza Sh20 milioni kwa wanamuziki 16,000 ambapo wa kwanza wanne walipokea zaidi ya Sh100,000.
Baadhi ya wanamuziki waliopokea donge nono ni Reuben Kigame na Denis Karanja Deno, wakipewa Sh122,741 kila mmoja.
Naye Joseph Ngala Katana alipewa Sh101,032 huku Solomon Mkubwa akipokea Sh74,138.
Nelly Wambui alipokea Sh52,000 na Milicent Jepkorir (Mali Safi) akipokezwa Sh108,123.
Mwaka 2023 baadhi ya wanamuziki kama vile Bien akiwa kwa kundi la Sauti Sol alitishia kujiondoa baada ya kutumiwa Sh14,634 na MCSK kwa njia ya M-Pesa.
Usambazaji huo ulimwacha kinywa wazi akishangaa jinsi ambavyo mwanamuziki Khaligraph Jones angepewa kiasi sawa na hicho.
Mwanamuziki na mchekeshaji Oga Obinna mwaka huo wa 2023 alitumiwa Sh258 pekee.