Shirikisho la Soka ‘TFF’ limesema Tanzania itakuwa kituo cha mafunzo ya mfumno wa VAR kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’.
Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred amesema kutokana na hilo wameanza kupata waamuzi watakaochezesha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON’.
“Kama nchi huwezi kutengeneza waamuzi wote bora, ila unaweza kupata waamuzi wanne ambao watakuwa wanawakilisha, hata huko Sudan hawaendi wote, ni wawili au watatu bora. Tumeanza kuona mafanikio kwani tumepata waamuzi ambao wameanza kuingizwa kwenye mchakato wa AFCON 2025.
“Kwa hiyo kuna kazi kubwa imeanza kufanyika kwa waamuzi wa kiume na wanawake. Jitihada nyingi zimefanyika kuwasaidia ikiwemo ujio wa mitambo miwili ya VAR, mmoja utakuwa Benjamin Mkapa na mwingine utakuwa unahamahama,” amesema Kidao.
Kuhusu Tanzania kutokuwa na waamuzi kwenye mashindano makubwa, Kidao amesema mwonekano wa mwamuzi, lugha ndio vitu vinavyofanya kukosa sifa na kuongeza kuwa wamekuja na mpango wa waamuzi vijana wenye vipaji ili kuondoa tatizo hilo.