Shime atamba kuiangamiza Afrika Kusini

Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’, Bakari Shime amesema maandalizi ya mchezo wa kutafuta nafasi ya kufuzu michuano ya Olimpiki dhidi ya Afrika Kusini yanaendelea vizuri na wana matumaini ya kufanya vizuri nyumbani.

Shime amesema wanatarajia kuwa na kambi ya siku 10 kabla ya mchezo na Afrika Kusini, ambao hautakuwa mchezo rahisi kutokana na aina ya wapinzani wao.

“Ndio kwanza tumeanza matayarisho yetu kwa wachezaji waliokuwa kwenye ligi na timu zao ndani na nje ya nchi, kazi ya kwanza ni kuangalia utimamu wa mwili na baada ya hapo tunaenda kuiunganisha timu yetu.

“Kikubwa ni kuhakikisha matayarisho yanaenda vizuri hatua kwa hatua na kuwa na kikosi imara na bora ambacho kitapata matokeo mazuri kwenye mchezo huu muhimu kwetu,” amesema Shime.

Amesema mchezo huu ni mkubwa kwani wamebakiza hatua mbili ili kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya Olimpiki kwa hiyo kikubwa kwao kama benchi la ufundi ni kuhakikisha kila kitu kinaenda vizuri.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii