Hugo Broos"Tulistahili kucheza fainali"

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ Hugo Broos amewapongeza wachezaji wake licha ya kushindwa kutinga Hatua ya Fainali ya Michuano ya Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ inayoendelea nchini Ivory Coast.

Bafana Bafana ilishindwa kujihakikishia kutinga Fainali ya Michuano hiyo itakayofikia tamati mwishoni mwa juma hili, kufuatia kufungwa kwa Penati 4-2 dhidi ya Nigeria, baada ya timu hizo kwenda sare ya 1-1 kwa dakika 120.

William Troost-Ekong aliipatia Super Eagles bao la kuongoza katika dakika ya 67 kutoka mkwaju wa Penati na ilipoonekana kana kwamba Wanigeria hao wangetinga kwa urafiki hatua ya Fainali, Afrika Kusini walipata Penati ikiwa imesalia dakika moja mpira kumalizika.

Teboho Mokoena wa Bafana alifanikiwa kuukwamisha mpira wavuni kwa mkwaju huo wa Penati na kuweka hai matumaini ya taifa lake.

Timu hizo mbili zilipata nafasi za kushinda katika muda wa ziada lakini zilishindwa kupata bao.

Baada ya mchezo huo, Broos alihisi timu yake ilikuwa bora zaidi huku akisema: “Kandanda inaweza kuwa ngumu. Ulioona mwenendo wa kikosi changu ​​halafu kuna Penati na unapoteza mchezo, hauko kwenye fainali, ni ngumu kukubali, kwa sababu tulicheza mchezo mzuri sana.

“Nadhani tulikuwa timu bora zaidi kipindi cha kwanza, tulipata nafasi nzuri zaidi. Nigeria haikuwa na nafasi moja, hapana, hakuna. Kipindi cha pili, sawa, walipata nafasi chache na kufunga.

“Lakini basi tulibadilisha kitu kimbinu na tuliweza kurejea lakini dakika mbili kabla ya dakika 90 kumalizika tulipata tena nafasi tatu. Kwa hivyo kama tungeweza kufunga, tungekwenda fainali na sio Nigeria.” Kocha wa Bafana alisema.

Vijana wa Broos watarejea tena uwanjani Jumamosi (Februari 10) usiku watakapomenyana na DR Congo kuwania nafasi ya tatu, dhidi ya DR Congo iliyotolewa na wenyeji Ivory Coast.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii