Wachezaji Watano Simba Waugua Ugonjwa wa Red EyesKOCHA Mkuu wa Simba Abdalhek Benchikha ameahirisha mapumziko aliyowapa mastaa wa timu hiyo waliokuwa Taifa Stars, baada ya wachezaji watano aliokuwa nao mazoezini kupatwa na ugonjwa wa macho mekundu'Red Eyes'.

Hilo limefanyika kabla ya mechi ya Shirikisho (ASFC) dhidi ya Tembo FC jioni hii aliposhituka nyota wake watano kuwa hoi na ugonjwa huo na kukosa nguvu kazi kikosini kwake ilihali kesho Alhamisi timu hiyo inasafiri kwenda Kigoma kwaajili ya mechi ya Jumamosi dhidi ya Mashujaa.

Viungo Babacar Sarr na Abdallah Hamis, mabeki Hamis Kazi na David Kameta 'Duchu' pamoja na Kipa Ally Salim ndio walikuwa wameshikwa na ugonjwa huo hadi tunaingia mitamboni jioni.

Baada ya kuona hivyo, Benchikha alimueleza meneja wa timu hiyo awajumuishe kwenye safari ya kesho, Aishi Manula, Mohamed Hussein, Mzamiru Yassin na Kibu Denis ambao awali hawakuwa kwenye mipango ya kwenda Kigoma kuwavaa Mashujaa.

Licha ya Simba kufanya siri, Mwanaspoti linajua wanasikilizia hali ya wachezaji waliokumbwa na ugonjwa huo na kama watakuwa bado hawajapata nafuu kufika kesho basi wataachwa Dar es Salaam.

Msimu mmoja uliopita kuna balaa moja liliikumba Simba ikiwa kwenye maandalizi ya kucheza na Kagera Sugar ugenini, ambapo kikosi cha wekundu hao kilisafiri mpaka mkoani humo tayari kwa mchezo huo.

Kabla ya kuondoka tayari Simba ilikuwa na idadi ya wachezaji wachache waliokuwa wanaugua mafua makali na kikohozi na baada ya kufika Kagera siku moja kabla ya mchezo maambukizi hayo yaliongezeka kiasi cha kundi kubwa la wachezaji na hata maafisa wake kuugua.

Mchezo huo ulilazimika kusogezwa mbele baada ya Simba kuliripoti mapema hatua ambayo ilikaribia kuuweka mchezo huo kwenye mashaka ya kuchezeka ingawa baadaye mechi ikachezwa baada ya wachezaji afya zao kuwa sawa.


Ugonjwa wa macho, maarufu kwa jina la ‘red eyes’ umeathiri zaidi watanzania 5,359 katika mikoa 17 ikiwa ni ongezeko la wagonjwa 4,250 ndani ya siku zisizozidi kumi. Watalaamu wanasema asilimia 80 mlipuko huo husababishwa na kirusi cha ‘Adenovirus’.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya afya zilizotolewa siku Januari 30, mwaka huu, kwa Dar es Salaam pekee, idadi imepanda kutoka 869 hadi 4,792 ndani ya wiki mbili.

Pamoja na Jiji la Dar es Salaam, mikoa mingine ni Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Katavi, Kilimanjaro, Mara, Iringa, Njombe, Ruvuma, Simiyu, Mtwara, Lindi, Songwe, Rukwa na Mwanza.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii