Aliyewahi kuwa Mchezaji na Kocha wa Simba SC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amemwagia sifa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha, kufuatia ushindi wa mabao 2-0 walioupata katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam juzi Jumanne (Desemba 19).
Ushindi huo umeifanya Simba SC ifikishe alama tano na kukaa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B nyuma ya vinara ASEC Mimosas yenye pointi 10.
Julio amesema mbinu zilizofundishwa na Benchikha ndio zilizoamua mechi hiyo ambayo matokeo yake yamefufua matumaini ya Simba kusonga mbele katika michuano hiyo ya kimataifa.
Beki huyo wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi pia alisifu kiwango kilichoonyeshwa na winga raia wa Cameroom, Essomba Onana, ambaye alipachika mabao yote mawili katika mechi hiyo.
“Kwa muda mfupi tu ameibadilisha Simba SC na kama atapata muda mrefu itakuwa timu ya kutisha zaidi, sio Tanzania, bali Afrika nzima, kuifunga Wydad Casablanca si jambo jepesi, ndugu zangu hizi timu za Waarabu siyo za mchezo mchezo, ni timu ngumu na nzuri ambazo mara nyingi zinachukua hivi vikombe vya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho,” amesema mchezaji huyo wa zamani wa Simba SC aliyeitumikia klabu hiyo kati ya mwaka 1980 hadi katikati ya 1990.
Ameongeza anaamini Simba SC itarejea katika ubora wake na kuwa tishio kwa sababu ya ujio wa kocha huyo mkongwe hapa barani Afrika.