Mapato chanzo anguko la Uongozi Mnada wa Pugu

Kushindwa kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato kwa Viongozi wa Mnada wa Pugu ni moja ya sababu iliyompelekea Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega kumuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Daniel Mushi kuuondoa madarakani uongozi mzima wa mnada huo.

Waziri Ulega alitoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika mnada huo mapema Januari 3, 2024 kwa lengo la kukagua na kubaini changamoto zinazowakabili Wafanyabiashara wa mnada huo.

Akitoa maamuzi hayo, alisema, “Naibu Katibu Mkuu ondoa uongozi mzima wa hapa mnadani, kuanzia Msimamizi Mkuu na wengine wote, leta watu wengine na hao wengine utakaowaleta uwape miezi sita kisha uniletee taarifa kama wanakidhi viwango.”

Kufuatia tukio hilo, pia alimuagiza Naibu Katibu Mkuu kuhakikisha anakagua minada yote mikubwa kukagua vyema utendaji wa minada hiyo na achukue hatua, ili kuboresha shughuli za sekta ya mifugo hapa nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Stesheni, Shukuru Mwinjuma alitaja changamoto ya wafanyabiashara wadogo kukamatwa na mifugo yao isivyo halali licha ya kuwa na vibali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii