Yanga na Msuva Mambo Safi, Kumtangaza Rasmi Mapinduzi Cup

Hatima ya winga wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Simon Msuva, kurejea katika klabu yake ya zamani ya Yanga huenda ikajulikana kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayotarajiwa kuanza kesho Visiwani Zanzibar, huku nyota huyo akisema lolote linaweza kutokea. Taarifa zilizopatikana jijini, Dar es Salaam zinasema Msuva ameshaachana na JS Kablie ya Algeria, na sasa yuko huru kujiunga na klabu nyingine.


Uamuzi wa kutangaza usajili wa nyota huyo huko Zanzibar ulitolewa na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, ambaye pia alikariri klabu yake itamtambulisha mchezaji ambaye si mgeni hapa nchini katika mechi yao ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi.


Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema tayari wameshakamilisha mazungumzo na nyota huyo ambaye yuko nchini akifanya mazoezi na kikosi cha Taifa Stars na kinachosubiriwa ni wakati huo sahihi waliopanga.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii