Wakurugenzi wawili wasimamishwa kupisha uchunguzi

Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, amewasimamisha kazi Wakurugenzi wawili wa Halmashauri kuanzia jana November 20, 2023 ili kupisha uchunguzi.


Wakurugenzi hao ni Butamo Nuru Ndalahwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Mkoani Morogoro Lena Martin Nkaya.

Hatua hiyo imekuja baada ya kupokea taarifa ya awali ya timu iliyoundwa kuchunguza tuhuma za Wakurugenzi hao kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo katika Halmashauri zao kwa nyakati tofauti, timu hiyo iliyoundwa na Katibu Mkuu kwa maelekezo ya Waziri Mchengerwa imebaini mapungufu ikiwemo kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo.

Mchengerwa amewasimamisha kazi kwa kuzingatia Kanuni ya 37 (1) na 38 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 ili kupisha uchunguzi wa kina, pia amewasisitiza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao kikamilifu ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo ambapo amesema hatosita kuchukua hatua stahiki kwa atakayethibitika kutenda kinyume.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii