Majanga yamuondoa Dalot kikosi cha Ureno

Beki wa Manchester United, Diogo Dalot amejiondoa kwenye kikosi cha Ureno kwa ajili ya mechi za kimataifa za mwezi huu.

Ureno maarufu kama ‘Selecao’ tayari wamejihakikishia nafasi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Ulaya ‘EURO 2024’ baada ya kushinda michezo yao yote nane ya kufuzu hadi sasa na watamaliza Kundi J kwa mechi za Ugenini huko Liechtenstein na nyumbani kumenyana na lceland juma hili.

Kocha, Roberto Martinez amefanikiwa kuiunda tena Ureno kama kikosi cha kushambulia, wamefunga mabao 32 katika mechi 12 za kufuzu ‘Euro 2024’, zaidi ya timu inayofuata lakini watalazimika kumaliza mechi zao mbili mwisho bila huduma hiyo ya Dalot.

United imethibitisha Dalot ameondolewa kwenye kikosi cha kimataifa cha Novemba kutokana na sababu kibinafsi na nafasi yake imechukuliwa na beki wa kulia wa FC Porto, Joao Mario.

Mwakilishi pekee wa Mashetani Wekundu katika maandalizi ya Martinez sasa ni nahodha wa klabu, Bruno Fernandes.

Kiwango cha Dalot katika ngazi ya klabu kuelekea dirisha la kimataifa kilishuka.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ameanza kila mechi kati ya mechi 10 za mwisho za United kwenye Ligi Kuu England, wakati mwingine akicheza kama beki wa kushoto kutokana na majeruhi wengi wa kikosi cha kwanza na kusababisha Erik ten Hag kukosa chaguo.

Licha ya mwanzo mbaya wa msimu huu, Dalot na wachezaji wenzake wa United walicheza mechi mfululizo za Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu kabla ya mapumziko ya kimataifa, wakishinda 1-0 Ugenini dhidi ya Fulham na nyumbani kwa Luton.

Mapema juma hili Man United ilifichua Christian Eriksen na Rasmus Hojlund pia wamejiondoa kwenye majukumu ya kimataifa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii