Malawi kuzuia baishara ya fedha za kigeni ili kunusuru uchumi

Malawi itaanza kuzuia biashara ya fedha za kigeni na kufanya msako dhidi ya wafanyabiashara magendo, baada ya kushuka thamani ya sarafu yake, wizara ya fedha imesema Jumatatu.

Kwa mujibu wa shirika la habari Reuters, nchi hiyo ya kusini mwa Afrika imeshusha thamani ya sarafu ya Kwacha kwa asilimia 30 dhidi ya dola ya kimarekani, Alhamisi, ikisema kwamba hatua hiyo ni muhimu katika kudhibiti wa soko la fedha.

Waziri wa fedha Simplex Chithyola Banda amesema Jumatatu kwamba mauzo ya fedha za kigeni kwenye benki pamoja na taasisi nyingine za kifedha hayatavuka dola 2,000 kuanzia sasa. Ameongeza kusema kwamba polisi wataanza kufanya miako dhidi ya wafanyabiashara haramu wa fedha, wakati alipokuwa akizungumza na wanahabari.

Amesema pia kwamba Malawi imeshauriana na Benki ya Dunia pamoja na mashirika mengine ya kimataifa kuhusu kuongeza misaada kwa watu masikini kupitia progam ya serikali ya Social Cash Transfer, SCTP, ili kuwalinda watu masikini dhidi ya athari za kushushwa kwa thamani ya sarafu, wakati pia kukiwa na mashauriano na mashirika ya wafanyakazi kuongeza mishahara.

Hii ni mara ya pili kwa Malawi kushusha thamani ya sarafu yake katika miaka ya karibuni, mara ya kwanza ilikuwa hapo Mei 2022. Hatua hiyo imepelekea malalamiko makali kutoka baadhi ya wakazi, ambao pia wanapanga kuandamana.

Bei za mafuta na umeme pia zilipandishwa Ijumaa iliyopita. Waziri wa fedha ametetea hatua hiyo akisema kwamba itasaidia kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa, pamoja na kuvutia wawekezaji wa kigeni.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii