CENI imepokea majina 24 ya wagombea urais kuelekea mchujo

Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imethibitisha kupokea orodha ya wagombea 24 wa urais ambao wamejisajili kuwania katika ucaguzi wa Desemba 20.

Licha ya orodha hiyo, wagombea bado wanahitaji kuidhinishwa na mahakama ya kikatiba kabla ya orodha kamili ya wagombea kuchapishwa tarehe 18 ya mwezi Novemba.

Rais Felix Tshisekedi, aliyeingia madarakani mwaka wa 2018, amewasilisha ombi la lake la kuwania katika uchaguzi huo mapema mwezi Oktoba, akiwania kuongoza DRC kwa awamu ya pili.

Kutokana na kile ambacho kimetajwa kwa mgawanyiko katika muungano wa upinzani, Tshisekedi mwenye umri wa miaka 60, amepewa nafasi ya kuibuka mshindi kwa mujibu wa mtaalam wa masuala ya kisiasa nchini humo Christian Moleka.

Upinzani wa kisiasa ambao umetajwa kugawanyika utahitaji kumuunga mkono  mgombea mmoja ili kupata nafasi ya kumshinda Tshisekedi, kulingana na Moleka.

Wapinzani wakubwa wa Tshisekedi ni pamoja na mshindi wa Tuzo ya Nobel Dkt Denis Mukwege, mfanyabiashara tajiri na gavana wa zamani wa Katanga Moise Katumbi, na Martin Fayulu, mgombea ambaye hakufanikiwa mwaka wa 2018.

Mbunge Delly Sesanga na mawaziri wakuu wa zamani Adolphe Muzito na Augustin Matata Ponyo pia wako kwenye kinyang'anyiro hicho, wa pili wakikabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu.

Kuna mwanamke mmoja pekee kati ya wagombea 24, Marie-Josee Ifoku Mputa, ambaye pia alishiriki katika uchaguzi wa 2018.

Hali ya kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ya sintofahamu kwa miezi kadhaa, huku vyama vya upinzani vikidai kuwa uchaguzi huo hautakuwa wa wazi.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii